Idara ya Vijana

1.0 UTANGULIZI

Idara ya Vijana na Wanafunzi ni moja ya Idara ya KKKT- Dayosisi ya Kaskazini. Idara ya Vijana na Wanafunzi inaratibu progamu zote za Vijana Sharikani, Vijana mashuleni na Vyuoni chini ya Ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania ( UKWATA) Mkoa wa Kilimanjaro na kuratibu shughuli za Liturjia na Uimbaji katika KKKT-Dayosisi ya Kaskazini. Lengo ni kuona vijana wanalelewa na kuwa na ustawi wa kiroho, kimwili, kiakili na kimaadili.

2.0 MADHUMUNI YA IDARA YA VIJANA NA WANAFUNZI

Idara ya Vijana na Wanafunzi ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini ipo kwa madhumuni yafuatayo:-

  • Kudumisha Umoja wa Vijana wote wa Dayosisi kwa kutiana na kupeana mawazo katika mambo mbalimbali yahusuyo maendeleo ya Vijana
  • Kuhimiza na kufundisha Vijana maadili mema ya Kikristo na Kijamii na hivyo kuwa watiifu na waaminifu kwa Kanisa na Taifa lao
  • Kutoa elimu ya mambo mbalimbali yahusuyo ustawi wa maisha yao na jamii kiroho, kiafya, kiuchumi, kiufundi na kielimu. Lengo ni kuwawezesha vijana kuinuka kiuchumi, kimaadili, kutumia muda wao vizuri, rasilimali zilizopo, kutunza mazingira, karama na vipawa vyao kwa halali, uzalendo kwa faida yao binafsi, taifa na kwa utukufu wa Mungu.
  • Kushauri na kuwasaidia vijana kuwa na uwezo wa  kuona fursa, kubuni miradi na  kupata mikopo kwa maendeleo yao.
  • Kufanya Uinjilisti kwa Vijana kwa njia za Uimbaji, Ziara, Ibada, Makongamano na hata kazi za Diakonia ndani ya eneo la dayosisi na nje.
  • Kuboresha mahusiano mazuri kati ya Vijana sharikani, majimboni na katika Dayosisi. Pia mahusiano mazuri baina ya Vijana na Uongozi wa Usharika, Jimbo, Dayosisi na nje ya Dayosisi.

3.0 VITENGO VYA IDARA YA VIJANA NA WANAFUNZI DAYOSISI YA KASKAZINI

3.1 USHIRIKA WA KIKRISTO WA WANAFUNZI TANZANIA (UKWATA)

Ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania (UKWATA) ni asasi chini ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) inayolenga kuwasaidia Wanafunzi wa Madhehebu ya CCT kiroho na kimaadili katika shule za Sekondari, Vyuo vya Ufundi ,Vyuo vya Elimu na Vyuo vingine vya Kanisa na vya Serikali.

Malengo Makuu ya UKWATA ni kuwasaidia Wanafunzi wawe na msingi bora wa maisha ya kiroho kwa njia za Ibada za pamoja,Vipindi vya kujifunza Biblia, Maombi, Sala. Chini ya UKWATA, Vijana Mashuleni huimarishwa kuiga tabia ya Yesu Kristo katika kudumisha Umoja, kuhudumiana kiroho  na kimwili wao kwa wao, pia kuwa na maandalio ya Kikristo na kutiwa moyo katika kulitumikia Kanisa.

KKKT Dayosisi ya Kaskazini ni Mlezi wa UKWATA katika Shule zote za Sekondari na Vyuo vyote vilivyo ndani ya eneo la Dayosisi.

3.2 LITURGIA NA UIMBAJI

Dayosisi ya Kaskazini kama sehemu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) linafuata Liturgia katika kufanya Ibada zake.Liturgia ni neno la Kiyunani lenye maana ya namna, mfumo au muundo wa kuongoza Ibada ulioandaliwa na Kanisa. Kwa kifupi neno Liturgia lina maana ya Ibada au utaratibu wa Ibada. Liturgia za kiprotestanti zinatilia mkazo katika kuhubiri na kufundisha Neno. Neno la Mungu ( Biblia) ndio lenye mamlaka ya juu na mwongozo sahihi wa mafundisho katika Kanisa; tofauti na mikazo ya baadhi ya madhehebu mengine yanayotegemea mafunuo, maono, hisia, sayansi n.k.

Mungu wetu ni wa utaratibu na ibada inapaswa ifanywe kwa uchaji na unyenyekevu.  Liturgia inatukumbusha kuwa tunapofanya Ibada tufanye kwa uchaji, utaratibu, kwa unyenyekevu, tukitubu makosa yetu, tukiabudu, tukimsifu, tukimshukuru, tukimwomba na kulisikia Neno lake.

Idara ya Vijana na Wanafunzi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Liturgia na Uimbaji ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini inao wajibu wa kuona Liturgia zinatunzwa ipasavyo na Uimbaji wa kitaalamu na unaomtukuza Mungu katika Kanisa unaimarika katika sharika zote za Dayosisi. Hili hutunzika kwa njia ya matamasha ya Uimbaji, Semina za liturgia na muziki wa Kanisa, Sikukuu za Uimbaji kwa ngazi za Sharika, Kanda, Jimbo na Dayosisi, Machapisho na miongozo mbalimbali yenye lengo la kutunza Liturgia na Muziki wa Kanisa.

3.3 VIJANA SHARIKANI

Vijana wameendelea kuwa kiungo muhimu cha Kanisa kwa ngazi za Sharika, Jimbo, Dayosisi na Kanisa zima. Sharika zote 164 za KKKT-Dayosisi ya Kaskazini zina Idara ya Vijana

Katika sharika Vijana wameendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali kama uimbaji, usafi wa mazingira, sanaa, miradi ya kilimo na Ufugaji, biashara ndogondogo wa msaada wa SACCOS hali kadhalika semina mbalimbali za kiroho, kimaadili na kiuchumi

3.3.1 WIKI YA VIJANA

Kila mwaka wiki ya Vijana huadhimishwa katika Dayosisi ya  Kaskazini kwa ngazi ya Usharika, Jimbo na Kidayosisi

Shughuli ambazo hufanyika katika wiki hii ni pamoja na kuotesha miti, semina za maadili na uchumi, kazi za udiakonia, usafi wa mazingira, michezo, ziara, kuongoza ibada siku ya kilele hali kadhalika sharika kufanya changizo maalum kwa miradi ya Vijana ya kidayosisi

3.3.2 NGARONY YOUTH CENTRE

Idara ya Vijana inaratibu mchakato wa kujenga  kituo cha Vijana Ngarony. Kituo hiki  kinajengwa na Dayosisi ya Kaskazini chini ya uratibu wa Kamati ya Ujenzi, katika eneo hili lenye ukubwa wa hekari 19 katika Kijiji na Usharika wa Ngarony-Jimboni  Siha kwa Malengo na Maono  yafuatayo:

i)   Kuwa Kituo cha kuwapatia Vijana mafunzo na mbinu za kuongoza wenzao katika Sharika na jamii kuhusu maendeleo ya Kiroho, kiuchumi na kijamii

ii)  Kituo kitakapokamilika kitakuwa ni mahali pa Vijana kujipatia maarifa kuhusu ujasiriamali na miradi ya kujikwamua na umaskini,utunzaji na uboreshaji wa mazingira, michezo na burudani

iii) Kuwapatia vijana stadi za maisha na mafunzo wakati wa kujiandaa kuanzisha unyumba kwa lengo la kuimarisha maisha ya familia.

iv) Kukutanisha Vijana wa eneo la Dayosisi na hata nje, kama wanaKanisa na wanajamii, kwa lengo la kufahamiana, kushirikishana mawazo na kuweka mipango ya pamoja ya kuchochea maendeleo yao, Kanisa na Jamii.

v) Kuwapatia Vijana eneo lenye mandhari nzuri kwa ajili ya mikutano na mikusanyiko yao.

vi) Eneo limekusudiwa kuwa na Ukumbi Mkubwa wa Mikutano, Nyumba ya Meneja, Hosteli za Vijana na Wageni, Jiko na Bwalo la Chakula, eneo la kukita mahema, vyoo na vyuma vya kuogea, Eneo la miradi ya mafunzo hali kadhalika maeneo ya michezo.

Fedha za kujenga kituo hiki inachangwa kwa juhudi za Vijana wenyewe ndani ya Dayosisi, Wanafunzi wa Jumiya ya Kikristo Tanzania (UKWATA), Sharika za Dayosisi, Harambee zinazoandaliwa na marafiki wenye wanaopenda maendeleo ya Vijana ndani na nje ya Dayosisi yetu.

3.3.3  VIJANA NA UIMBAJI

Idara ya Vijana huratibu na kufanikisha sikukuu ya Vijana na Uimbaji kila mwaka, lengo likiwa ni kuinua vipawa vya Uimbaji katika Sharika,Jimbo na Dayosisi na Uimbaji ulio na sura ya Kanisa

Hili hufanyika kwa njia ya Semina kwa Waalimu na Waongozavikundi vya  Kwaya, kuwa na Vikao vya Halmashauri ya Liturgia na Uimbaji kuanzia ngazi ya sharika, jimbo na Dayosisi, Kuandaa nyimbo za kitaalam na kuzituma kwa vikundi sharikani, kuwa matamasha ya Uimbaji na Sikukuu ya Uimbaji kwa ngazi ya Sharika,Jimbo na Dayosisi

3.3.4 UMOJA WA VIJANA

Idara ya Vijana inatia mkazo katika kujenga Umoja wa Vijana  wa Dayosisi na fursa za Vijana wa Dayosisi kukutana na kukaa na walezi wao kwa mafundisho, maonyo, ushauri na malezi

Pamoja na juhudi nyingine, Juma la Askofu na Vijana kila mwaka huwezesha Vijana kutoka kila Usharika wa Dayosisi ya Kaskazini kukutana kwa mafunzo, maphundo ya Kikristo, majadiliano, michezo na hata kujifunza katika mazingira wanakofanyia makusanyiko.

3.3.5 MICHEZO, MAZINGIRA NA HAKI ZA BINADAMU

Idara ya Vijana pia huhimiza Vijana kushiriki katika michezo mbalimbali, Utunzaji wa mazingira na utunzaji wa Haki za Binadamu.

4.0 CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI VIJANA

Changamoto zinazowakabili vijana bado ni kubwa kama ukosefu wa ajira, uvivu, ukosefu wa nafasi za elimu, ukosefu wa elimu ya kutoshakukata tamaa, ulevi wa pombe na madawa ya kulevyastaili mbovu za maisha zinazosukumwa na athari hasi za utandawazi,kutokuhudhuria ibadauzururaji, kutangatanga katika imani za madhehebu mbalimbali,tamaa ya fedha, ukosefu wa mitaji na mengine mengi yamewakabili vijana.

4.1 SULUHU YA CHANGAMOTO ZINAZOKABILI VIJANA

Suluhisho la changamoto zinazowakabili Vijana ni kama jamii na wadau mbalimbali wa Maendeleo kama serikali,  Mashirika yasiyo ya Kiserekali ( NGO’s), Kanisa na Vijana wenyewe wataweza kuona changamoto hizi na matokeo yake kisha kufikiri njia za kukabiliana nazo. Vijana wakitambuliwa, wakihamasishwa, kuwezeshwa na kupewa elimu na maadili bora katika maeneo yote na nyanja zote, tatizo litapungua kama si kwisha kabisa. Wachungaji na wote wanaopenda maendeleo ya Vijana wanao wajibu wa  kuhimiza Uinjilisti kwa vijana, huduma ya ushauri na utunzaji hali kadhalika kutenga muda wa Neno na Maombi na Vijana ikiwezekana mara moja kwa mwezi itasaidia sana kupunguza tatizo.

Idara ya Vijana na Wanafunzi  ya K.K.K.T Dayosisi ya Kaskazini inayo mikakati na mipango endelevu ya kutatua changamoto hizi na kuwafikia Vijana katika Sharika, Majimbo na eneo zima la Dayosisi kwa Ujumla.

Leave a Reply