Historia ya Dayosisi

askofu martin

K.K.K.T Dayosisi ya Kaskazini ina majimbo matano: Karatu, Siha, Hai, Kilimanjaro Kati na Kilimanjaro Mashariki. Pia inalea K.K.K.T. Dayosisi ya Konde, K.K.K.T Dayosisi ya Kusini Kati, na misioni ya Rukwa.  Pia kwenye umoja na dayosisi nyingine za K.K.K.T, imehusika kuanzisha na/ au kulea makanisa ya Kilutheri Congo DRC, Kenya, Malawi, Msumbiji, Rwanda, Uganda na Zambia.

Historia  Fupi K.K.K.T DK

Yohannes Rebmann, mmisionari Mlutheri Mjerumani, alizuru eneo la Kilimanjaro mara tatu kati ya mwaka 1847 na 1848, kama mjumbe wa Chama cha Misioni cha Kianglikana (Church Missionary Society) cha Uingereza. Alitokea Rabai, karibu na Mombasa, ambako Waanglikana wa CMS walikuwa wameanzisha kituo.

Ibada ya kwanza ya Kikristo kaskazini ya Tanzania ilifanywa na Waanglikana katoka mtaa wa Kitimbirihu,  Kijiji cha Mdawi, Old Moshi, tarehe 1 Julai, 1885, kwa mwaliko wa chifu Mandara (Rindi).

Wakati ule, mataifa ya Ulaya yaliafikiana kugawana Bara la Afrika.   Tanganyika ikatangazwa kuwa milki ya Wajerumani. Kwa hiyo, Waanglikana wakahamia Kenya, baada ya waamini wawili wa kwanza wananchi, Tomaso Ringo na Samueli Tenga kubatizwa, tarehe 21 Februari, 1892.  Baadaye, Chama cha Misioni cha Leipzig cha Ujerumani, kikaamua tarehe 8 Juni, 1892 kukitwaa kituo hiki.

Tarehe 30 Mei, 1893, wamisionari Wajerumani wanne, vijana, Gerhadt Althaus (26), Robert Fassmann (24), Emil Mueller (23) na Franz Boohme (23), walianza safari ya miezi minne kuelekea Kilimanjaro, ambako waliwasili tarehe 30 Septemba, 1893. Njiani, Italia, Mch. Traugott Paesler (43), aliyekuwa mmisionari Bara Hindi kabla, alijiunga nao kama kiongozi wa msafara.

kanisa

Siku zile, Chifu Meli, Mtawala Mpya wa Mochi, aliingia kwenye mzozo na Wajerumani.  Kwa hiyo wamisionari wakaamua kuelekea Nkwarungo, Machame, ambako waliwasili tarehe 2 Oktoba, 1893 na kupokelewa na Chifu Shangali na waliwekeana Mkataba ulioanzisha Nkwarungo- Machame, kama kituo cha kwanza cha Misioni ya Kilutheri Kaskazini ya Tanzania.

Hadi mwaka 1930, eneo pana la Kilimanjaro, Meru, Arusha na Pare lilikuwa na vituo 15 vya misioni. Tarehe 23-26 Agosti, 1930, wajumbe 50 kutoka vituo hivi walikutana Kotela, Mamba na kuunda Kanisa la Kilutheri la Afrika ya Mashariki. Miaka mitatu baadaye, Jumapili ya Epifania 1933, wananchi 15 wa kwanza walitumwa Machame kupata mafunzo ya theologia, chini ya Mch. Yohannes Raum na Mch. Dk. Bruno Gutmann na kubarikiwa kuwa wachungaji mwezi Mei 1934.

Mwaka 1942, katiba ya Kanisa hili ilifanyiwa marekebisho yaliyozaa Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kaskazini, likiongizwa na Mch. Dk. Richard Reusch, aliyejulikana kama Superintendent. Miaka mitano baadaye, Mch. Dk. Elmer Danielson alikabidhiwa wadk mushidhifa, akiwa na wasaidizi wawili, Mch. Solomon Nkya na Mch. Lazarus Laiser.

Tarehe 1 Februari, 1959, Mch. Stephano R. Moshi alisimikwa kuwa mkuu wa Kanisa, Msaidizi wake akiwa Mch. Dk. Elmer Danielson ambaye mwaka uliofuata alimwachia Mch. Horst Becker wadhifa huo. Kanisa hili liliungana na Makanisa sita mengine ya Kilutheri nchini kuanzisha Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), tarehe 19 Juni, 1963.  Kanisa hili likabadilika kuwa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, ambayo imezaa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati (1972), KKKT Dayosisi ya Pare (1975) na KKKT Dayosisi ya Meru (1992).

askof2

 

 

 

 

 

 

Askofu Moshi alifariki dunia mwaka 1976.  Dk. Erasto N. Kweka alichaguliwa mwaka 1977 kuwa Askofu.  Alipostaafu mwaka 2003, Dk. Martin F. Shao alichaguliwa kuwa Askofu kuanzia mwaka 2004.

 

 

Leave a Reply