KIUMAKO Sekondari Yafunguliwa Rasmi

Jumamosi ya tarehe 13 October 2018, Mhe. Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo alifungua rasmi shule ya Sekondari KIUMAKO iliyopo jimbo la Kilimanjaro Mashariki sanjari na kugawa vyeti kwa wahitimu 20 wa kidato cha nne shuleni hapo ikiwa ni mahafali ya kwanza tangu shule hiyo ilipoanzishwa mwaka  2004.

Awali Shule ya Sekondari  KIUMAKO ilisajiliwa kama kituo cha elimu(Educational Centre) mwaka 2008 na kupata usajili rasmi  kama shule ya Sekondari mwaka 2014. Ilianza na wanafunzi 34 sasa inawanafunzi 65 wa kidato cha kwanza hadi cha nne.

KIUMAKO ipo chini ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini. Jina KIUMAKO ni matokeo ya ushirikiano kati ya sharika za Kirimeni,  Uuwo, maring’a na Kondiki.

Katika salam zake Mkuu wa Kanisa  na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Baba Askofu Dkt. F. Shoo aliwashukuru na kuwapongeza marafiki kutoka shirika la RAFIKI nchini Ujerumani kwa misaada mbalimbali waliojitolea tangu kuanzishwa kwa sekondari ya KIUMAKO.

Kadhalika Baba Askofu Shoo aliwaasa wahitimu hao  kuweka bidii katika masomo na kumcha Mungu ili waweze kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuwaharibia mipango yao katika  Maisha.